Zifahamu faida za ndizi mwilini. - Mwl Ndiku

Saturday, 4 February 2017

Zifahamu faida za ndizi mwilini.


TOFAUTI na vyakula vingine, ndizi zinafaida kubwa sana katika mwili wa binadamu. Kwa mujibu wa wataalamu wa lishe, ndizi zina virutubisho vya aina mbalimbali kama vile, protini, mafuta, kalishiamu, wanga, fosiforas, madini ya chuma, vitamin A,B,C na maji.

Ndizi zina faida zipi katika urembo? Chanzo cha nishati Ndizi zina uwezo wa kumeng’enywa kwa urahisi zaidi, tena zina nishati kubwa, sukari iliyomo katika ndizi ni chanzo kizuri sana cha nishati.

Hivyo naweza kusema kuwa ndizi ikiliwa ipasavyo itakusaidia kujenga mwili na misuli yako kwa ujumla. Husaidia kuondoa chunusi Chunusi ni miongoni mwa matatizo ambayo huwasumbua warembo wengi hususan wanawake.

Je, unafahamu kuwa ndizi mbivu zinaweza kukuondolea tatizo hilo? Kwa kuchanganya ndizi mbivu na maziwa na asali na kisha kuzisaga ili kupata urojo ambao utatumia kupaka kwenye maeneo yaliyoathirika, unaweza kuondokana kabisa na tatizo hilo.

Fanya hivyo kila siku na hakikisha unakaa na mchanganyiko huo kwa muda usiopungua dakika 30 hadi 40, kisha osha na maji ya baridi ikiwezekana yaliyopozwa na jokofu.

Ndizi katika ‘diet’ Ndizi zina nafasi kubwa sana kati kuongeza au kupunguza uzito, hivyo unaweza kutumia ikiwa unahitaji kupunguza ama kuongeza uzito wako.

Kwa wajawazito Ndizi ni chakula kizuri kwa wanawake wajawazito, kwani kina kiwango kikubwa cha ‘folic acid’ ambayo inaweza kufyonzwa kwa urahisi sana na kiumbe kilicho tumboni. Ikiwa mama mjamzito atatumia ndizi mara kwa mara ni wazi kuwa atakuwa mwenye muonekano mzuri na wa kuvutia.


Ni kinga dhidi ya magonjwa ya moyo, presha, vidonda vya tumbo, saratani ya figo, kukosa choo

Ndizi mbivu ni tunda ambalo linafahamika na kila mtu, lakini sina hakika kama watu wengi wanafahamu umuhimu na faida za tunda hili ambalo linapatikana kirahisi sana nchini. Bei yake ni kati ya shilingi 50 na 150 tu, kiwango cha pesa ambacho kila mtu anaweza kukimudu.

Iwapo ulikuwa hujui umuhimu wa kula ndizi mbivu, leo utalazimika kubadili mtizamo wako na kuziangalia ndizi kama tunda muhimu katika kuupa nguvu na kuulinda mwili wako dhidi ya maradhi hatari ambayo hayana tiba. Watu wa michezo pia wanapaswa kuliona tunda hili kuwa ni muhimu sana katika kuipa miili yao nguvu.

KINGA DHIDI YA SHINIKIZO LA DAMU NA MARADHI YA MOYO
Kwa mujibu wa utafiti wa kisayansi, ndizi ni chanzo kikubwa cha Potassium, madini ambayo ni muhimu sana katika kuweka shinikizo la damu mwilini katika hali yake ya kawaida (Normal Blood Pressure), na ufanyaji kazi mzuri wa moyo. Kwa kuwa ndizi moja ina wastani wa 467mg za madini aina ya Potasiamu na 1mg ya sodiamu (chumvi), ndizi moja tu kwa siku inaweza kukupa kinga ya maradhi ya shinikizo la damu na matatizo ya moyo.

Ukweli kuhusu vyakula vyenye kiwango kikubwa cha madini ya Potasiamu katika kushusha shinikizo la damu mwilini, umethibitishwa na tafiti nyingi za kisayansi. Kwa mujibu wa jarida moja la masuala ya afya nchini Marekani, zaidi ya Wamarekani 40,000 wa kike na kiume, walifanyiwa utafiti kwa muda wa miaka minne na ikagundulika kwamba watu wanaokula vyakula vyenye kiasi kikubwa cha madini ya Potasiamu na kirutubisho cha Fiber (Ufumwele), wako katika hatari ndogo ya kupatwa na kiharusi.

Aidha, utafiti mwingine uliofanywa na taasisi moja ya masuala ya tiba ijulikanayo kama Archives of Internal Medicine, ya nchini Marekani, pia ilithibitisha kwamba ulaji wa vyakula vyenye kiasi kikubwa cha ufumwele (fiber) kama vile ndizi, husaidia sana kutoa kinga dhidi ya maradhi ya moyo. Na katika suala hili, zaidi ya watu 10,000 walifanyiwa utafiti kwa muda wa miaka 19.

KINGA DHIDI Y VIDONDA VYA TUMBO
Kwa muda mrefu sana imethibitishwa kwamba ndizi ina virutubisho vyenye uwezo wa kupambana na asidi tumboni hivyo kutoa kinga dhidi ya vidonda vya tumbo (stomach Ulsers) na kutoa ahueni kwa mtu ambaye tayari ameathirika. Katika utafiti mmoja, ilkibainika kwamba mtu akila mchangayiko wa ndizi mbivu na maziwa freshi, huzuia utokaji wa asidi tumboni inayosababisha vidonda vya tumbo.

Kwa mujibu wa utafiti wa kisayansi juu ya suala hili, ndizi hutoa kinga na ahueni ya vidonda vya tumbo kwa njia mbili. Mosi: virutubisho vilivyomo kwenye ndizi huzipa uhai seli zenye kazi ya kutengeneza utandu ambao hutoa aina fulani ya urojo (mucus) unaotumika kama kizuizi dhidi ya asidi tumboni.

Pili: kuna virutubisho vingine kwenye ndizi ambavyo kwa kitaalamu vinajulikana kama ‘Protease’ ambavyo husaidia kuondoa bakteria tumboni ambao wanaelezewa kuwa ndiyo chanzo cha vidonda vya tumbo. Hivyo kama wewe hujaptwa na vidonda vya tumbo, kwa kula ndizi mara kwa mara unajipa kinga madhubuti na kama tayari umeathirika na vidonda, kwa kula ndizi utajipa ahueni kubwa.

NDIZI KAMA TIBA KWA WENYE MATATIZO YA CHOO
Ndizi ni muhimu sana katika kulainisha na kusafisha tumbo na kumuwezesha mtu kupata choo. Mbali ya kusaidia upatikanaji wa choo kwa wenye matatizo hayo, lakini pia hutoa ahueni kwa wagonjwa wa kipindupindu. Mtu aliyepatwa na kipindupindu hupoteza kiasi kikubwa cha madini ya Potasiamu, hivyo kwa kula ndizi ataweza kurejesha mwilini maidni yake yaliyopotea na kuupa mwili nguvu yake.

UIMARISHAJI WA NURU YA MACHO
Wakati ulipokuwa mdogo, bila shaka uliwahi kuambiwa na mama kuwa mtu akila karoti, atakuwa akiona vizuri. Bila shaka hakukosea, lakini sasa ukiwa mtu mzima unaambiwa kwamba ulaji wa matunda, ikiwemo ndizi, ndiyo kinga hasa dhidi ya matatizo ya kutokuona vizuri uzeeni. Utafiti wa hivi karibuni unaonesha kwamba ulaji wa matunda kwa wingi kila siku, hupunguza kwa asilimia 36 matatizo ya kutokuona vizuri kutokana na mtu kuwa na umri mkubwa.

KINGA DHIDI YA SARATANI YA FIGO
Utafiti wa hivi karibuni uliochapishwa na Jarida la Kimataifa la masuala ya Saratani (International Journal of Cancer) la nchini Marekani, umeonesha kwamba ulaji wa mara kwa mara wa matunda halisi, hasa ndizi mbivu, ni kinga madhubuti ya mwili. Zaidi ya wawake 50,000 wenye umri kati ya miaka 40 na 76 waliofanyiwa utafiti, ulionesha kuwa wale waliokula wastani wa milo 2.5 ya matunda na mboga kila siku, walipunguza hatari ya kupatwa na saratani ya figo kwa asilimia 40.

Baadhi ya vitamini na madini yaliyomo kwenye ndizi ni pamoja na Vitamini B6, Vitamin C, Potassium, Dietary Fibre na Mnganese. Hivyo utaona kwamba tunda la ndizi ni muhimu kwa sababu limesheheni vitamini na madini muhimu katika mwili wa binadamu. Kuanzia leo itazame ndizi kama tunda muhimu sana katika ustawi wa afya yako na ni kinga dhidi ya maradhi unayoweza kuyaepuka kesho kwa kula tunda hili kwa wingi leo!

No comments:

Post a Comment