Mfahamu wakala wa Shetani. - Mwl Ndiku

Sunday, 20 November 2016

Mfahamu wakala wa Shetani.

WAKALA WA SHETANI  NI  NANI?

Watu wengi wamo katika makanisa mbalimbali wakifundishwa mapotofu na viongozi wao waliojitolea kikamilifu kumtumikia shetani. Kwa unafiki Biblia hutumika na huku imani zao zimesimamishwa kwa mwovu ibilisi. Kwa kufanya hivyo roho za mabilioni ya watu hupotea pasipo matumaini,
Ø  Tito 1:16, “Wanakiri ya kwamba wanamjua Mungu, bali kwa matendo yao wanamkana; ni wenye machukizo, waasi, wala kwa kila tendo jema hawafai.”
Ingawa madai yao huonekana kuhusiana na Mungu, kimsingi dini ambazo hushindwa kutimiza haki itokanayo na Mungu, hao hawatokani na Mungu na kamwe hawamwakilishi hata kidogo. Badala yake Biblia huwaeleza kama miti izaayo matunda mabaya.
Ø  2Timotheo 3:5, wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao”
Hebu tuitazame chachu ya Mafarisayo na Masadukayo. (Mathayo 16:6), “Yesu akawaambia, Angalieni, jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.” [ Neno chachu limetumika katika Biblia likimaanisha dhambi au uovu]. “Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.” (Mathayo 5:20.) je! Katika makanisa ya leo kuna mtu anaweza onekana kuwa na haki inayozidi ile ya Waandishi  na  Mafarisayo? Jibu ni hapana. Haki ya watu wa leo ni  mbaya zaidi, na hata chachu yao inazidi  ile ya Mafarisayo na Masadukayo. Watu wa siku hizi ni taasisi mpya za Shetani. Yesu alitoa ishara za namna ya kuwagundua wakristo wa kweli na wale wauongo.

 “Mtawatambua kwa matunda yao” ( Mathayo 7:16,20; Yohana 7:24.) ndivyo ilivyo, dini ya kweli ya Kristo, nabii wa kweli ambaye huongea maneno ya Mungu, na ukristo bandia, na nabii ambaye hutabiri uongo na asiyeongea maneno ya Mungu, wote hao hutambulika kwa matunda yao. Kila mti usio zaa matunda utakatwa nakupwa katika moto.

Je! Watu hao ni akina nani?
Wafuatao ni baadhi ya wazaa matunda mabaya          [ wasiotokana na Kristo na wafundishao mafundisho ya uongo]  wanaopatikana katika dini bandia ya kikristo.

“Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.” Mathayo 7:15-23.



SIFA ZA WAKALA WA SHETANI!
1.NI MPINGA KRISTO
Mmekwisha sikia kwamba mpinga Kristo anakuja, hata sasa wapo wapinga kristo  wengi kama tujuavyo tuko nyakati za mwisho.
“Na kila roho isiyomkiri Yesu haitokani na Mungu. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani.” 1Yohana 4:3

Mpinga Kristo ni kauli inayomwakilisha mtu yeyote anayekana fundisho au mafundisho yanayohusiana na Kristo, na pia wale wote walio kinyume na Kristo katika matendo yao. Dini zote katika ulimwengu zinadai kuwa zinamwabudu Mungu wa Ibrahimu. Baadhi zina kitu kimoja kinachofanana. Zinakana asili ya Kristo, kwamba Yeye si Mwana wa pekee wa Mungu aliyeumbwa kipekee na hili huwafanya kuwa wapinga Kristo.  Wanaamini kwamba wakati  jina “Mwana wa Mungu” likitumika kumwakilisha Kristo, inakuwa katika mfano au maelezo kama ya Mungu kumwita Israeli mzawa wake wa kwanza. Wanachoshindwa kutambua ni kwamba; maelezo na mfano “Mwana wa Mungu” aliumbwa na Mungu. (Luka 3:38; 6:35; Ayubu 1:6; Warumi 8:14-17), Yesu hawezi kuwa Mungu na Mwana wa Mungu. Kwa kuamini kwamba Yesu ni Mwenyezi Mungu wanaishia kumkana kuwa siyo Mwana wa Mungu. Walimwengu wote waendao  kinyume na jinsi Biblia  ielezavyo na wanaotegemea uwezo wa Shetani ni wapinga Kristo.

Hivyo basi kauli ya “MPINGA KRISTO” humlenga/huwalenga hawa wafuatao;
Ø  Wale wanaomkana Baba na Mwana_[1Yohana 2:22; tazama                    2 Wakorintho 1:3.]
Ø  Wale wanaoamini kuwa ‘Yesu hakuja katika mwili’_[ 2Yohana 1:7]
Ø  Wale wanaowapinga na kuwatesa wafuasi wa Kristo_ [Yohana 15:20,21; Luka 21:12.]
Ø  Yeyote asiye upande wa Kristo “Mtu ambaye si pamoja nami yu kinyume changu” [Luka 11:23.]
Ø  Yeyote anayejitangaza kuwa ni  MASIHI na manabii wa uongo_[Mathayo 24:24]
Ø  Waasi (Wale walio achana na ibada ya kweli)_[1 Yohana 2:18,19.]
Ø  Mnyama na sanamu yake [uasi wa Shetani katika siasa na serikali za ulimwengu], mataifa yanayompinga Kristo kama mfalme, au yanayo jikweza kuchukua nafasi ya Masihi_ [Zaburi 2:2; Ufunuo 19:19-21.]
Hao wote hapo juu ni wapinga Kristo na ndio mawakala wa shetani.

2.KUKUFURU
Je! Kukufuru ni kufanyaje? Ni tendo gani mtu akitenda  atakuwa amekufuru? Maandiko yanasemaje!!
Ø  Yohana 10:33, ― “Wayahudi wakamjibu, Kwa ajili ya kazi njema hatukupigi kwa mawe; bali kwa kukufuru, na kwa sababu wewe uliye mwanadamu wajifanya mwenyewe u Mungu.”

Ø  Marko 2:7, ― “Mbona huyu anasema hivi? Anakufuru. Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa mmoja, ndiye Mungu?”

Kutokana na neno la Mungu [Biblia] matendo haya mawili humaanisha kukufuru;
Ø  Mwanadamu kujifanya ni Mungu.
Ø  Mwanadamu kumwondolea dhambi mwanadamu mwenzake.

“Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi….” 2Timotheo 3:2

Kimsingi mtu anaye kufuru huutangazia ulimwengu kuwa Mungu hayupo na huwafanya watu kutatanika huku wakiitafuta njia ingawa wengi hupotea moja kwa moja. Usalama pekee ni kufuata Biblia inayomfunua Kristo kama mwokozi wa maisha yetu  kuliko kuamini mafundisho yaliyotungwa na  viongozi wako yasiyo patikana hata kwenye neno la Mungu [Biblia].

3. KUADHIMISHA SIKUKUU ZA KIPAGANI.
Hili ni jambo ambalo mamilioni ya watu wamekuwa mawakala wa shetani bila kujua. Mambo mengi ya kipagani yanatendeka katika makanisa ya leo ambapo hata ukiuliza wanatenda hivyo kwa andiko lipi, hakuna majibu utakayo pata kutoka katika Biblia. Baadhi ya mambo hayo ya kipagani ni pamoja na Christmas, pasaka za kila mwaka zinazotanguliwa na ijumaa kuu, siku ya wapendanao [valentine day], siku za kuzaliwa,  na mambo mengine yaliyoingizwa makanisani kutoka upaganini. Maandiko yanasema,

“..ujiangalie, usije ukanaswa ukawafuata, wakiisha kuangamizwa mbele yako; wala usije ukauliza habari za miungu yao, ukisema, Mataifa haya waitumikiaje miungu yao? Nami nifanye vivyo.” Kumb 12:30-32  … “Nanyi msiende kwa kuziandama desturi za taifa, niitoayo mbele yenu; kwa kuwa wao waliyafanya mambo hayo yote, na kwa ajili ya hayo niliwachukia.”  Walawi 20: 23.

Ndugu yangu kuwa wakala wa shetani maana yake ni kwenda kinyume na  maagizo ya Mungu na kufuata maagizo ya viongozi wa makanisa ambao kimsingi hupokea maagizo hayo kutoka kwa shetani nakuja kuwateka watu wayafuate ili Shetani atukuzwe.
Hebu tuaangalie vyanzo vya sherehe hizo zilizokuwa kawaida za washenzi au wapagani ambazo leo mamilioni ya watu wanaziamini;

A) Christmas – ni siku ambayo wakristo bandia kiunafiki wanadai kusherehekea kuzaliwa kwa Kristo . Christmas, ambayo ndiyo siku kuu kuliko zingine,  ina mizizi yake katika kuabudu jua. Tarehe 25 Desemba, ni siku ambayo tayari ilikuwa ikiadhimishwa na watu wa Rumi kama sherehe ya “Saturn” [mungu wa kirumi] ambapo wao zaidi walisherehekea kuzaliwa kwa “Mithras” mungu jua. Sasa hii siku ikachukuliwa na kutumika kama siku ya kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu kwa kadri walivyokuwa wakifanya upagani wao. Tena siku hiyo licha ya kuwa ni ya kipagani, lakini pia imeingizwa kwa uongo na udanganyifu. Kwa sababu hakuna mahali popote katika Biblia panapoonesha kuwa Mariamu alijifungua mtoto [ Yesu] tarehe 25 Desemba. Kwa hiyo wanatenda maovu kwa jina la Yesu; je! Tumaini lao ni lipi? Wakiendelea kuwa mawakala wa Shetani kwa kufuata mafundisho maovu na ya kipagani,  wasipo tubu na kumgeukia Mungu, hakika watapotea milele.

B) PASAKA [EASTER] – “Eastre” ni ‘mungu mke’ waliyemtegemea kuwapatia rutuba na maji ambapo kwa sasa tayari kuna mwunganiko wa upagani na ukristo.  Easter [siku ya ufufuo] imechukua jina la “mungu mke”  wa “Anglo-Saxon Teutonic” na dada wa Baal. Kwa hiyo namna inavyofanyika, taratibu zote, kimsingi wanakuwa wanamwenzi huyo mungu mke. Siku hii iliingizwa kwa kuwafumba watu kwa kuwadanganya kuwa ni siku ya kufufuka kwa Yesu. Lakini kiuhalisia ‘pasaka’ ni fundisho ovu lililofanikiwa kuwaangusha wakristo wengi kwa kuamini kuwa ‘ni siku ya ufufuo’. Je! Yesu anafufuka mara ngapi? Je! Ni wapi katika Biblia mitume na wafuasi wa Yesu waliadhimisha siku ya kufufuka kwa Yesu? Kama hakuna, wafanyao hivyo wamepata wapi?
 Ndugu yangu tafakali sana ufanye maamuzi sahihi kwa kuwa muda bado unao, maana wapo wengi wamekufa wakiamini uovo huo na huku walipata ukweli ila hawakuuamini kwa kuwaogopa wachungaji wao, hao hawana tumaini katika ufalme wa mbinguni, Kristo yu karibu kurudi kuwachukua wale wote waliofuata maagizo yake. Ole ni kwa wale waliofuata maagizo ya uongo [yasiyopatikana katika Biblia]. Ukimwuliza kiongozi wako wa kanisa  kuhusu mafundisho, akashindwa  kutoa majibu kutoka katika Biblia [neno la Mungu], ujue huyo ni wakala wa shetani na  ni  mwangamizaji wa Roho za watu.

C) SIKU YA WAPENDANAO [VALENTINE’S DAY] – Utaratibu huu wa siku ya wapendanao umetokana na sherehe ya Rumi ya kale iliyokuwa ikiitwa “Lupercalia” na ilikuwa ikifanyika kila tarehe 15 February. Warumi walikuwa na miungu mingi waliyo kuwa wanaitukuza  kama vile,  Juno, mungu mke.   Sasa huo ukafiri baadaye  ukaja kuiitwa kwa jina la kiongozi wa Katholiki aliyeitwa Valentine. Na  siku hii iliadhimishwa na warumi zama za kale ili kumpa heshima mungu wao wa mapenzi”, mwana wa Venus aitwaye  “Cupid”. Sasa upagani huo upo makanisani, je! tutapataje kupona?
 Lengo la Shetani ni kushusha kweli ya Mungu hadi chini, Danieli 8:12. Ili kukamilisha azima hiyo huwatumia watu [viongozi wa makanisa], kwa kupenda fedha na maslahi, viongozi hao huwateke akili waumini na kuwafumba macho wasione hatari inayo kuja. Sasa mafundisho ya uongo huingizwa kanisani kwa ujanja na kuwapotosha watu ili watawaliwe vizuri. Hao [wafundishao uongo] ni wakuogopa sana kuliko kitu chochote kile, kwa maana afundishaye uongo au aletaye fundisho lisilothibitika katika Biblia ili kupotosha Kweli ya Mungu, huyo ni mwuaji  wa  roho za watu “…mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum.” Mathayo 10:28.

D) KUADHIMISHA SIKU ZA KUZALIWA [BIRTHDAYS] – Utamaduni wa kuadhimisha siku ya kuzaliwa asili yake ni ushirikina uliokuwa ukifanyika hapo kale. Utamaduni huu wa kutoa hongera na zawadi ukiambatanishwa na kuwashwa mishumaa, hapo kale ulilenga  kufukiza miungu na kuomba ulinzi kwa mwaka unaokuja, na ndio maana huadhimishwa mara moja kwa mwaka. Huduma ya kuzima mishumaa ilifanywa na mungu mke [Artemis] wa Uyunani katika kila siku yake ya kuzaliwa. Kwa hiyo mishumaa iliwashwa juu ya keki kwa kuzunguka iliyoonekana kama mwezi, iliwekwa juu ya madhabahu. Mishumaa katika siku ya kuzaliwa, hapo kale ilimaanisha imani  ya  “kishirikina”  ya kumtakia mtu kila la heri.

 Onyo kwetu; Kumb 18:11,12 “….wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu. Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa Bwana; kisha ni kwa sababu ya hayo Bwana, Mungu wako, anawafukuza mbele yako.” 

Hadi sasa imani ya  ushirikina [uchawi] huo wa kusherehekea siku ya kuzaliwa, umeenea ulimwengu mzima; yaweza kuwa kuwaenzi waheshimiwa, taifa kusherehekea siku ya kupata uhuru, kukumbuka kuanzishwa kwa taasisi, hizo zote ni sanamu, hivyo, watu wanazidi kuleta mchukizo kwa Mungu.

E) MWAKA MPYA [NEW YEAR] –Watu wa Babeli mnamo karne ya 3 KK walianza kuadhimisha mwaka mpya ambapo wao waliifanya katikati mwa mwezi March. Inasemekana kuwa nyakati hizo mungu aitwaye “Marduk” alitoa mwelekeo kuhusu taifa kwa mwaka unaofuata. Mnamo mwaka 46 KK, mfalme mmoja mpagani aitwaye Julius Caesar alibadiri na kuamuru kuwa mwaka mpya utakuwa unafanyika ifikapo tarehe 1 January. Mpaka sasa imekuwa ndio msimamo wa kuadhimisha mwaka mpya kwa mataifa yote na kwa wakristo walioamua kuacha kweli ya Mungu na kufuata mapokeo. Kukubali mapokeo ya wanadamu ni kumpinga Kristo. Biblia inatwambia;
Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu,
  Ninyi mwaiacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu.” Marko 7:7,8.
 
4. KUCHANGANYA SIASA NA DINI
 Siasa ni sehemu ya ulimwengu, na dini ni  sehemu ya imani. Ulimwengu haukumtambua Kristo, bali wenye imani ya kweli ndio waliofuatana naye. Ndipo Yesu akasema, “… bali uwalinde na yule mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.” Yohana 17:15-16.
 Kanisa lolote likiungana na ulimwengu ni sharti likubaliane na matakwa ya ulimwengu. Hivyo ni lazima mafundisho ya kanisa hilo yafanane na ulimwengu [upotofu]. Kwa kuwa katiba za ulimwengu hupingana na Biblia Takatifu, viongozi wa makanisa asi kwa kutaka faidi na maslahi bila kuhurumia roho za watu, hubaki sasa wakitetea katiba za serikali za ulimwengu huku wakishusha kweli ya Mungu taratibu lakini kwa uhakika. Waumini hufumbwa macho kwa mafundisho yaletwayo na viongozi hao yalengayo kupotosha maagizo ya Mungu, hivyo hupotezwa bila huruma.
 Isaya  9:16, “Kwa maana wawaongozao watu hawa ndio wawakoseshao, na hao walioongozwa na watu hao wameangamia.”
Ndugu yangu usalama pekee si kujenga imani kwa kiongozi wa kanisa, jenga kwa Yesu mwamba pekee huku ukimwomba akumwagie Roho Mtakatifu akuongoze katika kujifunza Biblia, ndiyo njia ya kupinga viongozi waovu walio mawakala wa Shetani.
 
TUTAPATAJE KUPONA?
Ikiwa tunamtazamia Kristo arudi kutuchukua, swali hilo ni la msingi sana kwetu.
Biblia inatupa jibu, “…. Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.” Matendo 16:31.
Ulimwengu umejipaga kuleta mateso makali kwa watu wa Mungu. Maandiko yanatueleza dhiki hiyo ni ya muda mfupi tu ingawa atakaye vumilia hadi mwisho ndiye atakaye okoka. Je! Ni nani atakaye kuwa na nguvu za kuvumilia hadi mwisho?
Hapa ndipo penye subira ya watakatifu, hao wazishikao amri za Mungu, na imani ya Yesu.” Ufunuo 14:12
Biblia inawataja watakatifu kuwa wana sifa kuu mbili. Washikao “amri za Mungu” [Kutoka 20] na wenye “imani ya Yesu”[ Warumi 10:17].
Swali lingine la kujihoji ni kwamba, je! Kanisa ulilopo linatunza amri kumi za Mungu? Kwa maana kanisa litakalochukuliwa na Kristo ni lile lililotunza amri kumi za Mungu na likiwa na imani ya Yesu.

Hizi ndizo amri 10  za Mungu;
 Soma Kutoka 20:3-17.  
1. Usiwe na miungu mingine ila mimi.[Kutoka 20:3]

2. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia.……[Kutoka 20:4-6]

3. Usilitaje bure jina la Bwana, Mungu wako, maana Bwana hatamhesabia kuwa hana hatia mtu alitajaye jina lake bure.[Kutoka 20:7]

4. Ikumbuke siku ya Sabato uitakase……….. [Kutoka      20:8-11]

5. Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako.[Kutoka 20:12]

6. Usiue. [Kutoka 20:13]

7. Usizini. [Kutoka 20:14]

8. Usiibe. [Kutoka 20:15]

9. Usimshuhudie jirani yako uongo. [Kutoka 20:16]

10. Usiitamani nyumba ya jirani yako, usimtamani mke wa jirani yako; wala mtumwa wake, wala mjakazi wake, wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala cho chote alicho nacho jirani yako.[Kutoka 20: 17]

Kama tulivyoona hapo juu, mawakala wa shetani  nia yao kubwa ni kushusha kweli ya Mungu, watafanikiwa hata kubadili amri za Mungu na kuziweka kimakosa katika vitabu vingine vya kujitungia.
“…ataazimu kubadili majira na sheria…..;” Danieli 7:25.
Andiko hili limekwisha timia; Kwa mfano; watu mpaka sasa wanaamini kuwa amri ya nne ni “shika kitakatifu siku ya Mungu” badala ya “ikumbuke siku ya Sabato uitakase”. Swali ni kwamba, huyo anayesema shika kitakatifu siku ya Bwana, ametoa wapi? Ama kwa hakika huyo ndiye mpinga Kristo.
Katika kanisa la Mungu, mpendwa hutakuta sanamu, miungu wala mafundisho ya uongo. Maana yake ni kwamba kanisa hilo limejiandaa kumlaki Yesu.


Hatari kubwa ni hii;
Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni.” Mathayo 5 :19.

“Maana mtu awaye yote atakayeishika sheria yote ila akajikwaa katika neno moja, amekosa  juu ya yote. Kwa maana yeye aliyesema, Usizini, pia alisema, Usiue. Basi ijapokuwa hukuzini, lakini umeua, umekuwa mvunja sheria.” Yokobo 2:10-11.

Mpendwa, yawezekana umekuwa wakala wa shetani bila kujua, yawezekana umekuwa ukiaminishwa mafundisho ya uongo kwa muda mrefu na sasa umefahamu kuwa Mkristo wa kweli ni yule anayejifunza kutoka katika Biblia, hapunguzi wala kuongeza, ni heri sasa ufanye hima ili kukimbia maovu hayo ujiunge na walio tayari kutanga upendo na mahusia ya Yesu Kristo.
Ø  1Timotheo 1:13. “ingawa hapo kwanza nalikuwa mtukanaji, mwenye kuudhi watu, mwenye jeuri, lakini nalipata rehema kwa kuwa nalitenda hivyo kwa ujinga, na kwa kutokuwa na imani.”

Unapotafakali na kuchukua maamuzi bora kabisa kwa ajili ya roho yako, huku ukilenga kukimbia maovu ya hao mawakala wa shetani, Mungu akubariki na akuongoze katika kuiona njia ya uzima.

Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nawe siku zote. Amina.
Habari zaidi kuhusu masomo haya;
Namba, +255758924982, +255714697526. [Issaya]
E-mail ndiku.live@outlook.com

Facebook; Mwl Ndiku.

No comments:

Post a Comment