Namna ya kupata vifaranga vingi kwa mfugaji wa kuku. - Mwl Ndiku

Wednesday, 1 March 2017

Namna ya kupata vifaranga vingi kwa mfugaji wa kuku.


Kuna njia tofauti za kuanza au kuongeza mtaji kwa mfugaji wa kuku kama vile, kununua kuku 
wakubwa, vifaranga kutoka kwa wafugaji wengine au kuzalisha vifaranga wako wewe mwenyewe.

Kwa wafugaji wengi ambao wana lengo la kufuga kuku wengi wa umri mmoja na kupata mayai mengi au aweze kuuza kuku wengi kwa wakati mmoja wenye umri unaolingana inabidi uwe na vifaranga wengi wa umri mmoja.


Kwa nini kuwa na vifaranga wengi wa umri mmoja?

·                     Kupunguza gharama za ufugaji kwa mfano chanjo na tiba;
·                     Kutunza kuku kitaalam kwa urahisi
·                     Kupata mayai mengi kwa wakati mmoja
·                     Kuuza kuku wengi kwa waakti mmoja
·                     Kuwapa uhakika wateja wako


Hivyo kuna njia kuu mbili za upatikanaji wa vifaranga wengi kwa wakati mmoja nazo ni;
Kwa kuhatamiza kuku wengi kwa wakati mmoja


1.                  Kwa njia ya mashine ya kuangulia incubator)
2.                  Njia zote mbili huweza kutoa vifaranga bora bali uchaguzi wa njia ipi itumike utatokana na mtaji wa mfugaji na mahali alipo.


Kwa kuhatamiza kuku wenyewe
Njia hii hutumika kuhatamisha tetea wengi kwa wakati mmoja hivyo mfugaji anatakiwa achague mitetea, mayai, aandae viota, maji na chakula bora.

Sifa za tetea wa kuhatamia

·                     Kuku mwenye umbo kubwa
·                     Mwenye uwezo na historia nzuri ya kuhatamia na hatimaye kutotoa vifaranga


Sifa za mayai ya kuhatamisha

·                     Mayai ya siku ya mwisho kutagwa ndio yawe ya kwanza kuwekwa yafuatiwe na ya siku zinazofuata yasizidi wiki mbili tangu kutagwa
·                     Lisiwe kubwa sana au la duara, lisiwe na uvimbe
·                     Yasiwe machafu wala yasiwe na nyufa
Sifa za kiota na chumba cha kuhatamia

·                     Kuku wanaohatamia watengwe katika chumba ili kuondoa tatizo la kutagiana.
·                     Mlango na dirisha viwekwe wavu ili muda wa mchana mwanga na hewa uweze kuingia  ndani.
·                     Chumba kiwe na nafasi ya kutosha kuweka viota, chakula na maji.
·                     Ili kutumia eneo vizuri viota vinaweza kutengenezwa ukutani kama mashelfu.
·                     Viota viundwe vizuri kwa nyasi, maranda makavu ya mbao, au nguo ya pamba lakini isiyo tetroni.
·                     Viota visiwe sehemu yenye unyevunyevu.
·                     Idadi ya viota vilingane na idadi ya matetea walio chaguliwa kuatamia
·                     Vinyunyiziwe dawa ya kuuwa wadudu kama utitiri kwani hawa ni wadudu wasumbufu ambao husababaisha kuku kutokatoka nje, hivyo kupunguza uwezekano wa mayai kuanguliwa yote.

Chakula, vitamini na maji
Kuku wanaohatamia wapewe chakula cha kuku wakubwa wanaotaga (layers mash) cha kutosha muda wote kiwemo kwa kua kuku hawa hutoka wakati tofauti pia majani, mboga-mboga na maji ya kunywa ni muhimu sana. Vyote hivi viwekwe kwenye chumba ambacho kuku wanahatamia ili kumfanya kuku asiende umbali mrefu kutafuta chakula pia kuyaacha mayai kwa muda mrefu.

Hatua za kuhatamisha kuku
1.                  Kuandaa viota, uchaguzi wa matetea bora na kuandaa mayai.
2.                  Tetea wa kwanza akianza kuhatamia muweke mayai yasio na mbegu ama viza.
3.                  Rudia zoezi hili mpaka itakapo fikia idadi ya kuku unao wahitaji.
4.                  Baada ya kupata idadi ya kuku wawekee mayai yenye mbegu.


N.B. kuku wote waliochaguliwa kwa ajili ya kuhatamia wawekwe wakati wa usiku kwa sababu ya utulivu uliopo.

Kwa kupitia njia hii kuku mmoja anaweza kuhatamia hadi mayai 20 ukizingatia sifa za kuku huyo. Baada ya kutotoa hatua ya awali ya uleaji wa vifaranga. Kuku wazazi hutengwa na vifaranga ambapo vifaranga hupewa joto na mwanga kwa kutumia taa ya umeme, jiko au kandili. Maji yenye glucose kwa ajili yakuongeza nguvu, pia chakula.

Changamoto
·                     Huhitaji sehemu kubwa kwa sababu ili upate vifaranga wengi unahitaji kuku wengi wanao atamia.
·                     Kuwepo kwa wadudu kama utiriri na kutopatikana kwa chakula cha kutosha husababisha kuku kutoka toka nje na kusababisha mayai kuharibika.
·                     Kuku kupata magonjwa wakati wanapo atamia.
·                     Kutokuwa na kipimo cha kupimia mayai yaliyo na mbegu.
Ushauri kutoka kwa mfugaji: Wakulima tubadilike na kuanza kufuga kibiashara kwa kua soko la mazao ya kuku wakienyeji lipo. Pia tuweze kuzalisha mayai bora ya kutotolesha, ni muhimu sana yatokane na kuku wako ama kwa mfugaji ambaye una uhakika na ufugaji wake.

Nawatakia majukumu mema.


1 comment:

  1. vijana wengi mtaani tunapaswa kujiajiri badala ya kukaa bila kazi ya kufanya

    ReplyDelete