1.0 Utangulizi
Usimamizi wa Watumshi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa katika masuala ya upandishwaji vyeo, mafunzo na uhamisho yameelezwa katika Sheria ya Utumshi wa Umma Na 8 ya mwaka 2002, ikisomwa pamoja na Kanuni zake za mwaka 2003 na Taratibu za uendeshaji za mwaka 2003, pamoja na Miongozo na Nyaraka mbalimbali zilizotolewa na Serikali. Kwa sasa taratibu za kusimamia masuala hayo ni kama ifuatavyo:-
2.0 Kupandishwa Vyeo
Mamlaka ya kupandisha vyeo watumishi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa isipokuwa Walimu kwa mujibu wa Kanuni ya D. (f) na (g) ya Kudumu ya mwaka 2009 ni Halmashauri yenyewe.
2.1 Nini kifanyike kabla na baada ya mtumishi kupandishwa cheo?
- Mamlaka ya Ajira yaani Halmashauri inapaswa kutenga fedha na nafasi kwa ajili ya nafasi za vyeo vinavyaotakiwa kupandishwa kwa mujibu wa Miundo yao ya Utumishi na sifa za watumishi wanaotarajiwa kupandishwa vyeo.
- Mwajiri anapaswa kuhakikisha watumishi wake wanapimwa utendaji kazi kwa kutumia mfumo wa Upimaji na tathmini ya wazi �OPRAS� ili kujua hali ya utendaji wao. Mtumishi atakayezembea katika hili asipopandishwa cheo, halitakuwa kosa la mwajiri bali ni kosa la kiutendaji la mtumishi husika.
- Ukubwa kazini yaani elimu na uzoefu wa kazi pia ni kigezo muhimu katika kuwafikiria watumishi kupandishwa vyeo licha ya kuwa miundo ya utumishi iko kimya katika hili.
- Ni muhimu idhini ya kupandishwa watumishi vyeo baada ya Kamati za Ajira za Halmashauri kumshauri Mkurugenzi awasilishe taarifa kwenye Baraza la Madiwani la Halmashauri husika ili litoe idhini, vinginevyo vyeo vilivyopandishwa vitakuwa ni batili.
- Ni muhimu Vyama vya Wafanyakazi mahali pa kazi kupitia Mabaraza ya kazi vikashirikishwa katika maandalizi ya kupandisha watumishi vyeo ili kuepuka manung�niko yasiyo ya lazima mahali pa kazi.
- Ni muhimu kwa watumishi wote wa Mamalaka za serikali za Mitaa kufahamu kuwa nafasi zozote za kupandishwa vyeo hazitaombwa mpaka pale itakapolazimika Mwajiri kuzitangaza.
2.2 Taratibu za kujaza nafasi za Uteuzi
Katika utumishi wa umma kuna Taratibu na Miongozo inayotumika kujaza nafasi wazi na vyeo vya uteuzi. Taratibu hizo ni kama zilivyofafanuliwa hapa chini:-
- Nafasi za uteuzi zinapotokea katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kama ilivyo kwa taasisi zingine serikalini Waajiri watapaswa kutoa taarifa na mapendekezo ya maafisa wanaoweza kufikiriwa kushika nafasi hizo (majina yawe kati ya mawili na matatu) kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais -Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa hatua za upekuzi kisha baada ya kupokea majibu ya upekuzi, Mamlaka za uteuzi zitaendelea na uteuzi na kutoa taarifa za utekelezaji kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
- Pale inapotokea ni lazima nafasi za uteuzi ikaimiwe, kabla ya kupata kibali cha kukaimu nafasi hiyo, ni muhimu baada ya Mtumishi kukaimishwa na Mamlaka ya Uteuzi, Mamlaka hiyo kuomba kibali cha kuwakaimisha Watumishi wenye sifa za kukaimu na kupata kibali cha Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa umma kwa ajili ya malipo ya posho zao za kukaimu na kuwezesha zoezi la upekuzi kuendelea wakati wahusika wanakaimu.
- Mara baada ya watumishi kupandishwa vyeo Waajiri wanapaswa kuhakikisha kuwa watumishi wanapewa barua zao za kupandishwa vyeo na wanabadilishiwa mishahara yao kwa wakati bila kuzalisha madeni kwa Serikali.
- Mtumishi aliyepandishwa cheo atapaswa kuwa katika kipindi cha majaribio na atathibitishwa katika cheo alichopandishwa baada ya miezi sita tangu tarehe ya kupandishwa cheo.
- Iwapo itaonekana mtumishi ameshindwa kumudu majukumu ya cheo alichopandishwa atajulishwa na kupewa sababu na nafasi ya kujieleza kwanini asivuliwe cheo hicho na kulingana na maelezo hayo anaweza kuongezwa muda wa majaribio.
2.3 Nini kifanyike iwapo Mtumishi hajaridhika na utaratibu uliotumika kumpandisha cheo?
Iwapo mtumishi ataona hakutendewa haki na Mamlaka yake ya ajira katika suala la kupandishwa cheo atapaswa kuchukua hatua zifuatazo;
- Kumjulisha Mwajiri Malalamiko yake kwa barua,
- Iwapo Mtumishi hataridhika na majibu ya Mwajiri, atapaswa kutoa malalamiko yake kwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma kwa uamuzi ambapo nakala ya barua yake itatumwa Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
No comments:
Post a Comment