“Fumbua Macho Ewe Msafiri wa Kwenda Mbinguni”
Watu wengi wamo katika makanisa
mbalimbali wakifundishwa mafundisho ambayo hayathibitiki katika Biblia. Baadhi
ya viongozi katika makanisa hayo wanafahamu vizuri kuwa wanapotosha kondoo wa
Kristo, lakini kwa kutafuta faida na maslahi yao, huficha ukweli wa Mungu na
kufundisha mapokeo ya wanadamu.
Marko 7:7-8, “Nao waniabudu
bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu, Ninyi mwaiacha
amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu.”
Kwa unafiki Biblia hutumika na
huku imani zao zimesimamishwa kwa mwovu ibilisi. Kwa kufanya hivyo roho za
mabilioni ya watu hupotea kila kukicha. Tena maandiko husema;
Tito 1:16, “Wanakiri ya
kwamba wanamjua Mungu, bali kwa matendo yao wanamkana; ni wenye machukizo,
waasi, wala kwa kila tendo jema hawafai.”
Ndugu yangu mpendwa hebu leo
tuchunguze japo kwa ufupi mafundisho mapotofu ambayo watu wengi wameyajengea
imani. Kristo analo kanisa ambalo hakuna hata fundisho moja potofu
linalopatikana humo. Kanisa hilo limejengwa kwenye msingi wa mitume na manabii
na ni lenye kushika maagizo ya Mungu. Kanisa hilo hufundisha mafundisho ya
kibiblia na kukemea upotofu kama ilivyo elezwa hapo chini.
Fundisho la ubatizo.
Mathayo 28:19-20, “Basi,
enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba,
na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru
ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”
Agizo la Yesu Kristo ni kueneza
injili na kuwabatiza wale watakao amini kuwa Yesu ni Bwana na mwokozi wa
maisha yao. Ubatizo ni huduma ambayo watu tusinge leta mzaha kwa sababu kwa
kukiri ubatizo sahihi ni moja ya sharti ambalo kwalo twaweza kuuona ufalme wa
Mungu.
Yohana 3:3, “Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu
asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.”
Yohana 3:5, “Yesu akajibu,
Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia
ufalme wa Mungu.”
Kigezo cha kwanza katika
ubatizo ni kuamini. Pili ni lazima pawepo na maji. Je! Maji hayo
ni ya namna gani? Je! Ni ya kwenye bakuli au ya mtoni, ziwani na baharini?
Marko 1:4-5, “Yohana alitokea, akibatiza nyikani, na kuuhubiri ubatizo wa toba
liletalo ondoleo la dhambi. Wakamwendea nchi yote ya Uyahudi, nao wa Yerusalemu
wote, wakabatizwa katika mto wa Yordani, wakiziungama dhambi zao.”
Mathayo 3:13, “Wakati huo
Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka Yordani kwa Yohana ili abatizwe.”
Kwa mantiki hiyo mpendwa
ubatizo ni lazima uwe wa maji mengi na siyo kwenye bakuli yaani kunyunyiza
kichwani. Pia anaye batizwa awe na uwezo wa kuamini. Kumbe sasa mtoto
hapaswi kubatizwa kwa kuwa hajafikia fahamu za kuamini injili.Wale
wanao tazamia Yesu arudi kuwachukua wanapaswa kuzamishwa ndani ya maji ikiwa
ndio ubatizo sahihi ambao hata Kristo aliutumia.
Je! Ni kwa nini tunapaswa kuzamishwa ndani ya maji?
Warumi 6:4, “Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika
mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya
utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima”
Wakolosai 2:12, “Mkazikwa pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa
pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua katika wafu.”
1Petro 3:20-21, “watu
wasiotii hapo zamani, uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja, siku za Nuhu,
safina ilipokuwa ikitengenezwa; ambamo ndani yake wachache, yaani, watu wanane,
waliokoka kwa maji. Mfano wa mambo hayo ni ubatizo, unaowaokoa ninyi pia siku
hizi; (siyo
kuwekea mbali uchafu wa mwili,
bali jibu la dhamiri safi mbele za Mungu), kwa kufufuka kwake Yesu
Kristo.”
Kwa maandiko hayo mpendwa kubatizwa
kwa kuzamishwa ndani ya maji ni kukiri kuwa Yesu alikufa na akafufuka
katika wafu. Na kukubali kunyunyizwa maji kichwani, ni kupinga Biblia kuwa Yesu
hakufa nalo ni moja ya fundisho la mpinga Kristo. Kuna batizo nyingi kama vile
kuruka moto, kunyunyiza maji kichwani na hata kuvuka bendera; batizo hizo ndugu
yangu hazitambuliki mbinguni, ni ubatizo mmoja tu yaani kuzamisha ndani ya
maji ndio unaothibitika kimaandiko ambao Yesu na mitume waliutumia. Ana
heri yule ateteaye Maandiko Matakatifu kuliko yule ateteaye mafundisho ya
mchungaji wake.
Fundisho jingine linalopinga
Biblia ni la mwanadamu kuchukua mamlaka ya kumwondolea dhambi mwanadamu
mwenzake. Kwa kufanya hivyo ni kutangaza kuwa Mungu hayupo. Viongozi
wa madhehebu mengi huwalazimisha waumini wao kwenda kutubu dhambi mbele yao na
kusema yote waliyokosa. Jambo hili liko kinyume na mpango wa Kristo wa
kuukomboa ulimwengu kwa sababu watu wanaishia sasa kumwabudu mwanadamu
badala ya Mungu Mwenyezi. Yesu anasema;
Mathayo 11:27-28, “Akasema, Nimekabidhiwa vyote na baba yangu; wala hakuna
amjuaye Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana, na ye yote ambaye
Mwana apenda kumfunulia. Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye
kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.”
Isaya 1:18, “Haya, njoni,
tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana,
zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa
kama sufu”
Ndugu yangu iwapo umekosa au
una hatia ya kutenda dhambi usalama wako ni kupiga magoti na kutubu kwa Yesu
Kristo siyo kwenda kwa mchungaji au kiongozi wako wa kanisa. Kanisa la Yesu
ndilo pekee haliwezi kuruhusu mafundisho yasiyo ya kibiblia na liko tayari
kukemea mafundisho yote yasiyotokana na neno la Mungu, hata wewe waweza kuwa
mmoja wa kondoo halisi wa Kristo utakaefukuza giza la mafundisho maovu ikiwa
utaifuata njia nyembamba.
Giza lingine la kiroho ni
kuweka “wachungaji wa mishahara”. Ni kukosa wito wa kufanya kazi ya Yesu
na kuweka wachungaji wa vyeo ambao kimsingi huja kwa kuhitaji maslahi na kupitisha
mafundisho ya uongo na kuvutwa zaidi na mishahara na siyo mambo ya kiroho.
Maandiko yanasema;
Yohana 10:12-13, “Mtu wa
mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwa-mwitu
anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia; na mbwa-mwitu huwakamata na kuwatawanya.
Yule hukimbia kwa kuwa ni mtu wa mshahara; wala mambo ya kondoo si kitu
kwake.”
Uovu huo husababisha hata
kuwekwa kwa viwango vya zaka na sadaka na kuwalazimisha waumini watoe viwango
hivyo vya pesa waingiapo katika ibada ili kukidhi mishahara ya wachungaji.
Ndugu yangu ni muda wa
kujihoji, ikiwa kanisa ulilopo limekanyaga maandiko matakatifu au amri za Mungu
kwa kufuata faida za kidunia, fanya hima utoke ujiunge na kondoo wa Yesu kabla
muda haujakwisha maana Yesu anakuita ni vema kwako ukiitika.
Yesu yuko anabisha hodi katika
mioyo yetu, ikiwa tutaisikia sauti yake tukakimbia maovu na kushika maagizo
yake, basi tutakula mema ya nchi. Lakini tukishupaza shingo na mioyo na
kuwasikiliza viongozi wa wakanisa (watu wa kupenda mishahara), ole iko juu
yetu.
Ufunuo 18:4, “Kisha nikasikia
sauti nyingine kutoka mbinguni, ikisema, Tokeni kwake, enyi watu
wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake.
Neema ya Bwana Yesu na iwe
pamoja nanyi nyote. Amina.
Habari zaidi kuhusu masomo
haya;
Namba, 0758924982, 0714697526.
E-mail ndiku.live@outlook.com
Facebook; Mwl Ndiku.
No comments:
Post a Comment